Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Machafuko na ukiukaji mkubwa waendelea kuathiri raia Libya

Machafuko na ukiukaji mkubwa waendelea kuathiri raia Libya

Ripoti mpya ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, UNSMIL na Ofisi ya Haki za Binadamu, OHCHR, imesema kuwa Libya inaendelea kughubikwa na mgogoro wa kisiasa na machafuko makubwa katika maeneo kadhaa, na hivyo kuchangia kusambaratika kwa utawala wa sheria. Taarifa kamili na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Ripoti hiyo imesema kuwa pande zote katika mzozo nchini Libya huenda zinatenda uhalifu wa kivita, zikiwa zinakiuka sheria ya kimataifa ya kibinadamu na sheria ya kimataifa ya haki za binadamu.

Aidha, ripoti inabainisha hasa ukiukaji unaotekelezwa dhidi ya raia walio hatarini, mathalan wakimbizi wa ndani, watetezi wa haki za binadamu, wahamiaji, wasaka hifadhi na wakimbizi.

Mifano ya ukiukaji huo uliotekelezwa kati ya Januari mosi na Oktoba 2015, ni ushambuliaji holela wa maeneo yanayokaliwa na raia, utekaji wa raia, utesaji na mauaji holela, pamoja na uharibifu wa mali kwa kukusudia na ukiukaji mwingine mbaya wa sheria ya kimataifa.