Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yaonya dhidi ya usugu wa viua vijasumu

WHO yaonya dhidi ya usugu wa viua vijasumu

Shirika la Afya Duniani WHO limeeleza leo kwamba watu wengi duniani kote hawajaelewa hatari ya usugu wa viua vijasumu na hivyo kusababisha hatari kubwa kwa afya ya umma. Taarifa zaidi na Amina Hassan

(Taarifa ya Amina)

Hii ni kwa mujibu wa utafiti uliofanyika kwenye nchi 12 miongoni mwa watu zaidi ya 10,000, ukionyesha kwamba asilimia 75 ya watu hawajui kwamba usugu wa viua vijasumu unaweza kuathiri kila mtu, kwa sababu ni vimelea ambavyo vinakuwa na nguvu kinzani, wala si mwili wa binadamu.

Akizungumza na waandishi wa habari, mkurugenzi mtendaji wa WHO, Daktari Margaret Chan ameomba hatua thabiti zichukuliwe ili kubadilisha tabia za jamii, akisema:

(Sauti ya Bi chan)

“ Ongezeko la nguvu kinzani dhidi ya viua vijasumu ni mzozo wa kimataifa. Serikali nyingi zinatambua umuhimu wa tatizo hilo. Ni moja ya hatari kubwa ya afya siku hizi. Nguvu kinzani dhidi ya viua vijasumu inaongezeka kwenye kila sehemu duniani kote. Tunapoteza uwezo wetu wa kutumia aina ya kwanza ya kawaida ya viua vijasumu.”

Amesema tayari barani Afrika na Asia, mlipuko wa kifua kikuu wenye nguvu kinzani dhidi ya viua vijasumu unakumba maeneo kadhaa, huku nusu tu ya wagonjwa wakiweza kutibiwa.