Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ILO na hatua za G20 za kuondokana na ukosefu wa ajira zisizo na usawa

ILO na hatua za G20 za kuondokana na ukosefu wa ajira zisizo na usawa

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la kazi duniani, ILO Guy Ryder amesema hatua za kundi la 20 zenye uchumi mkubwa zaidi duniani katika kuondoa ukosefu wa usawa pahala pa kazi ni mwelekeo mzuri kwenye kuchagiza ukuaji uchumi jumuishi. Akizungumza kwenye kikao cha viongozi wa G20 kuhusu ukuaji jumuishi, Bwana Ryder amesema hatua hizo za mwezi Septemba mwaka huu ni pamoja na kuimarisha mifumo ya kupanga kiwango cha ujira na kupigia chepuo ajira bora.

Hata hivyo amesema hatua hizo ni lazima ziende sambamba na mikakati ya kifedha ili kusaidia kuinua vipato vya kaya za kiwango cha chini na kati.

Amesema uwekezaji pia kwenye miundombinu ni muhimu kama nchi ya kuweka fursa za ajira na kuongeza tija. Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa ILO, ukosefu wa usawa makazini unachochewa na ujira uliodumaa, ukosefu wa uhakika wa ajira na ongezeko la ajira za muda.