Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuelekea COP21 wakati ni sasa kulegeza misimamo:Ban

Kuelekea COP21 wakati ni sasa kulegeza misimamo:Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameonya kuwa hatua za kundi la nchi 20 zenye uchumi mkubwa zaidi duniani, G20 kuhusu mabadiliko ya tabianchi zinaweza kuleta mafanikio au changamoto zaidi kwenye kujenga dunia salama na endelevu.Taarifa kamili na Grace Kaneiya.

(Taarifa ya Grace)

Amesema hayo huko Antalya, Uturuki kwenye mkutano wa kundi hilo wakati huu ambapo zimesalia wiki mbili kuanza kwa mkutano wa COP21 wa kupitisha makubaliano mapya ya mabadiliko ya tabianchi huko Paris, Ufaransa.

Ban ametolea mfano suala la uwiano tofauti katika uwajibikaji wa nchi na uchangiaji fedha kwa mujibu wa kiwango cha uchafuzi ambapo amesema hilo ni suala lililozua mkwamo ambalo viongozi wa G20 wanapaswa kuwapatia mwongozo wawakilishi wao kwenye mazungumzo tangulizi ya Paris.

Ban amesema muda umekwisha na wakati huu ambapo dunia inaelekeza macho kwa viongozi hao ni vyema wakatoa mwongozo wa kisiasa utakaosaidia wawakilishi wao kukamilisha kazi kwa kulegeza misimamo na kufikia maridhiano.

Kundi la nchi 20 linachangia zaidi ya asilimia 75 ya gesi chafuzi duniani.