Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya watu milioni 2.6 wamefurushwa makwao eneo la Ziwa Chad

Zaidi ya watu milioni 2.6 wamefurushwa makwao eneo la Ziwa Chad

Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu katika Umoja wa Mataifa, OCHA,  imesema kuwa zaidi ya watu milioni 2.6 wamelazimika kuhama makwao katika nchi nne za ukanda wa Ziwa Chad tangu Mei 2013 kutokana na machafuko yanayoenezwa na kundi la kigaidi Boko Haram.

Takwimu za hivi karibuni zaidi za OCHA zinaonyesha kuwa takriban watu milioni 2.2 kati ya milioni 2.6 waliolazimishwa kuhama wanaishi ndani ya Nigeria, huku laki nne wakiwa wamelazimika kuvuka mipaka na kukimbilia nchi za Cameroon, Niger na Chad.

Kwa mujibu wa OCHA, zaidi ya watoto laki mbili hawaendi shule kwani zaidi ya shule elfu moja, ama zimeharibiwa au zimefungwa.

Kwa ujumla, watu milioni tano wanahitaji msaada wa chakula, huku watoto laki mbili wakiwa na utapiamlo. Toby Lanzer ni Mratibu wa Kibinadamu ukanda wa Sahel

"Ni eneo ambako watu milioni 25 hawana uhakika wa chakula na watu milioni tano wanakumbwa na njaa. Kadhalika kuna takriban watoto 700,000 ambao watafariki  kwa ajili ya utapiamlo katika ukanda wa Sahel"