Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Serikali zapaswa kuimarisha usalama barabarani: Ban Ki-moon

Serikali zapaswa kuimarisha usalama barabarani: Ban Ki-moon

Leo ikiwa ni siku ya kukumbuka wahanga wa ajali za barabarani duniani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesisitiza kwamba licha ya kuimarika kwa usalama barabarani, bado dunia inakumbwa na idadi kubwa ya vifo na majeraha yaliyosababishwa na ajali za barabarani.

Kwenye ujumbe wake kwa siku hii, Katibu Mkuu ameziomba serikali kuimarisha sheria za kudhibiti tabia za kuendesha magari kwa kasi kubwa, kulewa au kutotumia kanda za usalama ambazo zinasababisha ajali nyingi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, watu wapatao milioni 1.25 wanafariki duniani kila mwaka kutokana na ajali za barabarani, ajali hizo zikiwa ni sababu ya kwanza ya vifo vya vijana wenye umri wa kati ya miaka 19 na 25.

Wakati huo huo Shirika la Afya Duniani WHO linaandaa kongamano la ngazi ya juu kuhusu usalama barabarani wiki hii nchini Brazil.