Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua dhidi ya ugaidi zapaswa kuheshimu haki za binadamu

Hatua dhidi ya ugaidi zapaswa kuheshimu haki za binadamu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema hatua zitakazochukuliwa dhidi ya ugaidi uliokumba Ufaransa, Lebanon na Misri hivi karibuni zinapaswa kuheshimu haki za binadamu na utawala wa sheria, vinginevyo hatua hizo zitachochea ghasia zaidi.

Amesema hayo akizugumza na waandishi wa habari mjini Antalya, Uturuki, wakati wa mkutano wa nchi ishirini zenye utajiri mkubwa zaidi, G20.

Katibu Mkuu ameongeza kuwapa pole raia wa Ufaransa katika wakati huu wa msiba na masikitiko baada ya mashambulizi ya ijumaa nchini humo.

Aidha ameeleza kwamba ni lazima kupambana na mizizi ya itikadi kali, akisema kwamba anatarajia kuwasilisha mbele ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa mpango kazi wa kupambana na itikadi kali.