Mashambulizi ya kigaidi Lebanon yalaaniwa na Umoja wa Mataifa

Mashambulizi ya kigaidi Lebanon yalaaniwa na Umoja wa Mataifa

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amelaani vikali mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea tarehe 12, Novemba kwenye maeneo ya Burj al-Barajneh yaliyo karibu ya mji mkuu wa  Lebanon, Beirut.

Kwenye taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Bwana Ban amenukuliwa akieleza kusikitishwa sana na idadi kubwa ya wahanga, huku akituma salamu zake za rambirambi kwa familia za wahanga na kuwatakia nafuu majeruhi.

Aidha ameomba waliotekeleza uhalifu huo wapelekwe haraka iwezekanavyo mbele ya sheria.

Kwa upande wake Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu nchini Lebanon Sigrid Kaag amelaani mashambulizi hayo yaliyosababisha vifo angalau 40 na zaidi ya majeraha 200, akisema pande zote nchini Lebanon zinapaswa kutunza usalama na utilivu wa nchi hiyo.