Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maelfu ya maisha ya wahamiaji na wakimbizi yapotea wakisaka hifadhi: UNHCR

Maelfu ya maisha ya wahamiaji na wakimbizi yapotea wakisaka hifadhi: UNHCR

Licha ya mazingira hatari baharini, idadi ya wakimbizi na wahamiaji wanaowasili nchini Ugiriki hususani kisiwani Lesvos inaongezeka ambapo kwa sasa imefikia wastani wa 3,3000 kwa siku katika mwezi Novemba.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR linasema kati ya wakimbizi na wahamiaji zaidi 600,000 ambao wamewasili Ugiriki mwaka huu, nusu yao wamefika kisiwani Lesvos huku wakikabiliwa na changamoto kadhaa zikiwamo majira ya baridi kali yanayotarajiwa punde na uwezo finyu wa kuwahifadhi.

Kwa mujibu wa UNHCR, hadi sasa katika mwaka huu wa 2015 zaidi ya wahamiaji 3,000 wamefariki dunia katika bahari ya Mediterranean, 360 kati yao wakifariki ndani ya mwezi mmoja .

UNHCR imesema inafanya kazi na kikosi cha ulinzi katika Pwani nchini Ugiriki kupeleka vifaa zaidi vya uokozi na tayari imeshatoa vifaa vya kusaidia katika zoezi la uokozi linaloendelea.