Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa Valletta ni hatua muhimu, lakini kazi ndiyo sasa yaanza- UNICEF

Mkutano wa Valletta ni hatua muhimu, lakini kazi ndiyo sasa yaanza- UNICEF

Shirika la Kuhudumia Watoto, UNICEF, limesema kuwa mzozo wa sasa wa wakimbizi na wahamiaji ni onyo kuhusu changamoto za kiuchumi na kijamii zinazowaathiri watoto na vijana barani Afrika, na ambazo haziwezi kuendelea kupuuzwa.

Ikikaribisha matokeo ya mkutano wa Valletta ambapo viongozi kutoka Ulaya na Afrika waliafikiana kuhusu mpango wa hatua zinazoweza kuchukuliwa, UNICEF imesema kuwa kushughulikia mizizi ya uhamiaji wa watu Afrika kunahitaji kuangazia moja kwa moja watoto na vijana.

Mkurugenzi wa Ofisi ya UNICEF katika Muungano wa Ulaya, EU, Noala Skinner, amesema viongozi wa Ulaya na Afrika waliokutana Valletta walitambua kuwa kuwapa matumaini vijana na kuwalinda watoto kutokana na ukatili na unyanyasaji popote walipo, iwe majumbani, safarini au nchi wanakohamia, ni muhimu katika bara la Afrika ambako takriban nusu ya idadi ya watu ni watoto.

Wakati huo huo, Msimamizi Mkuu wa Shirika la Mpango wa Maendeleo, UNDP, Helen Clark, amesema kuumaliza mzozo wa uhamiaji Ulaya kutahitaji ushirikiano kwa upana baina ya nchi na mashirika ya kimataifa katika kushughulikia vyanzo vya uhamiaji wa halaiki, huku zikiwekwa njia zaidi za watu kuhama kisheria.