Skip to main content

Tume ya haki za binadamu DRC yajengewa uwezo

Tume ya haki za binadamu DRC yajengewa uwezo

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC warsha ya kimataifa inaendelea kwa ajili ya kuimarisha tume ya kitaifa ya haki za binadamu iliyoanzishwa nchini humo mwezi Aprili mwaka huu.

Warsha hiyo iliyoandaliwa kwa ushirikiano na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu nchini humo imeleta pamoja wanachama wa tume ya kitaifa, wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, wanaharakati wa haki nchini DRC na wataalam wawili kutoka Burundi.

Akizungumza na Radio Okapi mjini Kinshasa, DRC, Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu nchini DRC José Maria Aranaz amesema lengo la warsha hiyo ni kujenga uwezo wa tume ya kitaifa kupitia mifano ya tume zilizobobea barani Afrika, kama vile Burundi, Afrika Kusini au Togo akisema ni muhimu kuona kwamba nchi zingine zimeshakabiliana na changamoto zinazoikumba tume ya DRC.

“ Lengo letu kubwa ni kuwa na tume ya kitaifa yenye nguvu na uhuru, itakayotambuliwa rasmi kwa kiwango cha A kwa ngazi ya kimataifa, na itakayoaminika na taasisi za serikali lakini hasa raia wa DRC.”

Amesema tume hiyo changa bado inapaswa kuimarika ili kuweza kufuatilia kesi zote za ukiukaji wa haki za binadamu zinazotokea nchini humo, huku akitaja ukwepaji sheria, haki za watu wenye ulemavu wa ngozi, haki za kijamii na kiuchumi au uhalifu wa kijinsia.