Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mzozo Burundi, baraza la usalama lachukua hatua

Mzozo Burundi, baraza la usalama lachukua hatua

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio kuhusu Burundi, ambalo pamoja na mambo mengine linaelezea azma yake ya kuzingatia hatua zaidi dhidi ya  pande zote kwenye mzozo huo ambazo vitendo au kauli zao zinaweza kuchochea kuzorota zaidi kwa usalama na kukwamisha kupatikana amani.

Azimio hilo namba 2248 limepitishwa wakati wa kikao cha dharura kilichoitishwa kutokana na kuendelea kuzorota kwa hali ya usalama nchini humo huku mauaji ya raia yakiripotiwa kila uchao.

Aidha azimio hilo pamoja na kutambua hatua za msuluhishi wa mzozo huo, Rais Yoweri Museveni wa Uganda pia limesihi serikali ya Burundi kumpatia ushirikiano ili kuweza kupatia suluhu ya kudumu.

Halikadhalika limekaribisha uamuzi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon wa kuteua mshauri maalum kuhudu udhibiti wa mizozo ikiwemo Burundi.

Mwakilishi wa kudumu wa Uingereza kwenye Umoja wa Mataifa Matthew Rycroft ambaye ni Rais wa Baraza la usalama kwa mwezi huu wa Novemba anasema..

(Sauti ya Balozi Rycroft)

“Azimio la leo ni hatua moja muhimu mbele, na inatuma ujumbe wa pamoja wka pande zote nchini Burundi kushiriki kwenye mazungumzo na kujiepusha na ghasia. Ishara hii inapatiwa uzito zaidi na tamko la pamoja lililotolewa na Muungano wa Ulaya, Muungano wa Afrika na Umoja wa Mataifa.”

Hata hivyo wajumbe kupitia azimio hilo wamemtaka Katibu Mkuu afuatilie kwa karibu hali ya Burundi na wamemshauri apelike timu nchini humo itakayoshirikiana na serikali, Muungano wa Afrika na wadau wengine kutathmini wasiwasi wa kisiasa na usalama nchini humo.

Na kwa mantiki hiyo wamemtaka Katibu Mkuu ndani ya siku 15 alipatie Baraza hilo tathmini ya hali ilivyo ikiwepo mustakhbali wa uwepo wa Umoja huo nchini Burundi.