Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM watoa dola milioni 17 kusaidia walioathirika na ukame Ethiopia

UM watoa dola milioni 17 kusaidia walioathirika na ukame Ethiopia

Mratibu Mkuu wa masuala ya kibinadamu katika Umoja wa Mataifa, Stephen O’Brien, ametoa leo dola milioni 17 kutoka Mfuko wa Jitihada za Dharura wa Umoja wa Mataifa, CERF, kuwasaidia watu walioathiriwa na hali ya ukame nchini Ethiopia, ambayo ndiyo mbaya zaidi katika miongo kadhaa iliyopita.

Fedha hizo za CERF zitasaidia katika kutoa bidhaa muhimu za chakula kwa watu walioathiriwa na ukame kwa wakati huu na pale wanapozihitaji.

Hali ya hewa ya El Niño imeathiri mvua za msimu wa jua kali nchini Ethiopia, baada ya kutokuwepo mvua msimu uliotangulia baada ya kumalizika msimu wa baridi kali. Hali hiyo imeongeza hali ya kutokuwa na uhakika wa chakula, utapiamlo na uhaba wa maji katika maeneo yaloathiriwa nchini.

Akitoa fedha hizo, Bwana O’Brien amesema jitihada za mapema ni muhimu, na kuonya kwamba hatua zisipochukuliwa sasa, huenda kukaibuka hali mbaya zaidi kesho, mahitaji yakiwa makubwa zaidi mwaka 2016.