Mkuu wa UNHCR apongeza nia ya Ban kumteua Grandi kuongoza shirika hilo

12 Novemba 2015

Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR Antonio Guterres amekaribisha tangazo la Katibu Mku wa Umoja wa MAtaifa Ban Ki-moon la kutaka kumteua mwanadiplomasia mwitaliano Filippo Grandi kuwa mrithi wake kwenye UNHCR .

Kwenye taarifa iliyotolewa leo, Bwana Guterres amenukuliwa akisema kwamba Bwana Grandi ni kiongozi anayeheshimika sana na mwenye uzoefu mkubwa wa kimataifa kuhusu swala la ukimbizi.

Tayari Rais wa Baraza Kuu Mogens Lykketoft ameeleza kuarifiwa na Katibu Mkuu Ban kuhusu nia yake ya kumteua Grandi kushika wadhifa huo wa juu kwenye UNHCR na kusema kuwa wiki ijayo ataitisha kikao cha Baraza Kuu kwa ajili ya uchaguzi wake.

Grandi amekuwa Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia wakimbizi wa Palestina UNRWA tangu mwaka 2010 hadi 2014. Amewahi pia kufanya kazi nchini Kenya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo miongoni mwa nchi nyingi zingine.

Mwezi ujao UNHCR itatimiza miaka 65 tangu kuanzishwa kwake ikiwa sasa na wafanyakazi zaidi ya 9,000 na ikihudumia wakimbizi zaidi ya milioni 60 duniani kote.