Mratibu wa kibinadamu Libya akaribisha kuachiliwa kwa waliotekwa
Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu nchini Libya, Ali Al-Za’tari, amekaribisha kuachiliwa kwa wahudumu wawili wa kibinadamu baada ya miezi mitano matekani, na kuwashukuru wote waliosaidia katika kuhakikisha raia hao wa Libya wanaachiliwa.
Mohamed al-Monsef Ali al-Sha’lali na Walid Ramadan Salhub walikuwa wanapeleka misaada kusini magharibi mwa Libya walipokamatwa mnamo Juni 5, 2015 huko al-Shwayrif, kusini mwa nchi.
Wanaume hao waliokuwa wanafanya kazi na shirika la kibinadamu la Shaik Tahir Azzawy – ambalo husaidia mashirika kadhaa ya kimataifa katika kutekeleza shughuli zao – waliachiliwa huru mnamo Novemba 7, 2015.Akieleza kufurahishwa na kurejea kwao wakiwa salama kwa familia zao, Bwana Ali Al-Za’tari, amesisitiza haja ya kuwezesha usambazaji wa misaada ya kibinadamu kwa njia salama kote nchini, akiongeza kwamba kuwafikishia misaada wenye uhitaji kunapaswa kulindwa na kutoathiriwa na migogoro.