Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Benki ya maziwa ya mama ni moja ya mbinu bunifu za kuondokana na numonia:

Benki ya maziwa ya mama ni moja ya mbinu bunifu za kuondokana na numonia:

Ikiwa leo ni siku ya homa ya vichomi au numonia duniani, shirika la afya WHO kwa kushirikiana na wadau wake limetaja hatua tano muhimu za kuzuia na hata kutibu ugonjwa huo  ambao unsalia kuongoza kuua watoto wengi zaidi kwenye nchi zinazoendelea.

Mbinu hizo tano zimetajwa katika tovuti maalum kwa siku hii ambapo ya kwanza ni chanjo ya pneumococcus ambayo imeelezwa kuwa  ingawa na aghali, ubia kati ya sekta binafsi na  umma unaweza  kurahasisha upatikanaji wake.

Pili ni teknolojia rahisi kupitia simu za mkononi ambayo huwezesha kupima kiwango cha hewa ya oksijeni mwilini, Iwapo mtu anaugua numonia kiwango hicho hupungua na hivyo kubaini mapema kunawezesha tiba mapema.

Tatu ni antibayotiki ambayo ni rahisi kwa watoto kuitumia kwa kuwa baadhi yao hushindwa kumeza vidonge. Tovuti hiyo inataja mbinu ya nne kuwa ni kuhakikisha nyumba ni safi na haina hewa nzito.

Mbinu ya tano ni benki ya maziwa ya mama ambapo wanahamasisha wanawake kujitolea maziwa yao ambayo hatimaye yatahifadhiwa na kuweza kupatiwa watoto wachanga waliokosa maziwa ya mama.

Kwa mujibu wa WHO miaka 15 iliyopita watoto Milioni mbili walifariki dunia kila mwaka kutokana na numonia lakini kutokana na mbinu bunifu, idadi hiyo sasa imepungua lakini bado hatua zaidi zahitajika.