Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kampuni za kimataifa hukwepa ushuru kwenye nchi zinazoendelea: ECOSOC

Kampuni za kimataifa hukwepa ushuru kwenye nchi zinazoendelea: ECOSOC

Umuhimu wa ukusanyaji ushuru kwa ajili ya kufadhili uwekezaji wa kitaifa na maendeleo umemulikwa leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York ambapo kumefanyika mkutano maalum kuhusu ukusanyaji wa mapato ya taifa.

Mwenyekiti wa kamati ya pili ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Andrej Logar amesema mapato hayo ni muhimu na hivyo ili kuhakikishia utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2030, ni lazima kuimarisha mifumo ya ukusanyaji ushuru.

Kwa mantiki hiyo amekumbusha kuwa suala hilo lilikuwa ni moja ya nyenzo za kuongeza ufadhili wa maendeleo zilizobainishwa wakati wa kongamano la kimataifa lililofanyika mjini Addis Abeba nchini Ethiopia mwaka huu kuhusu ufadhili kwa maendeleo.

Hata hivyo Bwana Logar ameeleza kwamba bado changamoto zipo, ikiwemo uwezo wa taasisi zinazohusiana na ukusanyaji ushuru kwenye nchi zinazoendelea, akisema kuwa ni asilimia moja tu ya usadizi wa kimataifa wa maendeleo unalenga kujenga uwezo wa taasisi hizo.

Kwa mantiki hiyo ameomba jamii ya kimataifa iongeze jitihada zake kwani zinaweza kuleta mafanikio makubwa katika maendeleo.

Kwa upande wake Rais wa Baraza la Uchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa Oh Joon amesisitiza kwamba ukusanyaji wa ushuru unapaswa kuangaziwa kwa ngazi ya kimataifa kwa sababu kampuni nyingi zinakwepa ushuru kwenye nchi zinazoendelea, huku akieleza kwamba hadi dola bilioni 240 za ushuru kutoka kwa kampuni kubwa za kimataifa zinapotea kila mwaka.

Amesema pesa hizo zingenufaisha zaidi nchi zinazoendelea na hivyo Bwana Oh Joon amesema suluhu ni..

“ Ushirikiano mkubwa zaidi baina ya nchi. Wanaokwepa au kukimbia ushuru wanastawi iwapo kuna pengo la ushirikiano wa kimataifa na ukosefu wa taarifa baina ya nchi. Kwa hiyo ni muhimu kwa manufaa ya serikali zote kushirikiana ili kupambana na vitendo vibaya vya ukwepaji ulipaji ushuru. »