Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban afunguka kuhusu mipango ya kupunguza misaada ya maendeleo

Ban afunguka kuhusu mipango ya kupunguza misaada ya maendeleo

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesema kuwa wakati dunia ikikabiliwa na mzozo mkubwa zaidi wa watu kulazimika kuhama makwao tangu vita vikuu vya pili vya dunia, jamii ya kimataifa ikabiliane na changamoto hiyo kubwa bila kupunguza usaidizi wake rasmi kwa maendeleo.

Akishukuru jamii katika nchi zinazowahifadhi watu waliolazimika kuhama makwao kwa ukarimu wao na serikali zinazotoa usaidizi, Ban amesema anatambua mahitaji ya kifedha zinazokabiliana nayo jamii hizo na serikali katika kutoa usaidizi huo.

Aidha, Katibu Mkuu amesisitiza umuhimu wa kufadhili kikamilifu juhudi za kuwasaidia wakimbizi na waomba hifadhi katika nchi wanakokimbilia, pamoja na juhudi za muda mrefu za maendeleo, akisema kuwa kuelekeza rasilimali katika sehemu moja kusimaanishe kukomesha ufadhili kwa nyingine.

Ban ameonya kuwa kutofadhili usaidizi wa maendeleo kwa wakati huu kunaweza kuendeleza kuwepo kwa changamoto ambazo jamii ya kimataifa imejitoa kukabiliana nazo, na kukwamisha juhudi za kuboresha fursa za afya, elimu na maisha bora kwa mamilioni ya watu kote duniani.