Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuanguka kwa bei ya mafuta kunautia uchumi wa Iraq matatani- Kubis

Kuanguka kwa bei ya mafuta kunautia uchumi wa Iraq matatani- Kubis

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu na Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq, UNAMI, Jan Kubis, ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa kuanguka kwa bei ya mafuta kimataifa kumeongeza wasiwasi kuhusu uchumi wa Iraq, ambayo inakabiliwa na upungufu katika bajeti yake na matatizo ya kiuchumi.

Kwa mantiki hiyo, Bwana Kubis amesema kuna haja ya kufanya mabadiliko ya dharura katika uchumi wa taifa hilo.

Natoa wito kwa serikali ya Iraq na kwa wadau wa kimataifa, zikiwemo taasisi za kiuchumi za kimataifa na za kikanda, kuchukua hatua za dharura kushughulikia changamoto zinazotoa shinikizo za kiuchumi na za bajeti”

Kuhusu maridhiano ya kitaifa nchini humo, Bwana Kubis amesema, licha ya matumaini kuwa Waziri Mkuu Haider al-Abadi angeweza kusongesha harakati za maridhiano mbele na kuijumuisha jamii ya Sunni katika mchakato wa kisiasa, juhudi zake zimekumbana na vizuizi kutoka pande zote za jamii ya Iraq, sababu kubwa ikiwa ni kutoaminiana na maslahi ya kibinafsi.

Hata hivyo, wengi wa raia wa Iraq wanaamini kuwa Waziri Mkuu al-Abadi ndiye anayewezesha kuwepo Iraq bora zaidi, migawanyo michache kwa misingi ya dini, yenye ufanisi zaidi, na wanamuunga mkono. Waziri huyo Mkuu bado anaungwa mkono kisiasa na kiongozi mwenye ushawishi mkubwa, Ayatollah al-Sistani na Marja’iya”

Kuhusu kazi ya UNAMI, Bwana Kubis amesema ujumbe huo umeendelea na juhudi zake za kuendeleza maridhiano ya kitaifa miongoni mwa viongozi pande zote Iraq, taasisi za kiraia, jamii mashinani na katika nchi jirani, kwa kushirikiana na serikali ya Iraq.