Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Licha ya kucheleweshwa, uchaguzi waandaliwa nchini CAR

Licha ya kucheleweshwa, uchaguzi waandaliwa nchini CAR

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, MINUSCA, umefuraishwa na kutangazwa rasmi kwa ratiba ya uchaguzi nchini humo, ukisema ni hatua muhimu katika utaratibu wa mpito.

Kwa mujibu wa mkuu wa idara  ya uchaguzi wa MINUSCA, Bouah Mathiew Bile, aliyehojiwa na radio ya MINUSCA Guira FM, kura ya maoni kuhusu katiba itafanyika tarehe 13, Disemba, huku awamu ya kwanza ya uchaguzi wa rais na wabunge ikitarajiwa kufanyika tarehe 27 mwezi Disemba mwaka huu.

Bwana Bile amesema kwamba licha ya kuahirishwa, uchaguzi umeonyesha utayari wa raia wa CAR kupiga kura, huku watu milioni 2 wakiwa wameshajiandikisha kwenye orodha za kupiga kura.

(Sauti ya Bwana Bile)

"Nadhani uchaguzi umecheleweshwa kidogo tu, na uongozi wa kisiasa unasimamia utaratibu huo, kwa sababu licha ya siasa, kuna masuala ya kitaaluma. Lakini msingi wa utaratibu wa uchaguzi ni utashi wa kisiasa. Uchaguzi utafanyika kwenye mazingira magumu lakini angalau utashi wa kisiasa upo, pia dhamana zote zinazohitajika na uelewa wa kila mtu."