Skip to main content

Baraza la Usalama lakutana kuhusu Bosnia na Herzegovina

Baraza la Usalama lakutana kuhusu Bosnia na Herzegovina

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo limekuwa na mkutano kuhusu Bosnia na Herzegovina, ambapo pia limepitisha kwa kauli moja azimio la kuongeza muda wa kikosi cha kuweka utulivu kinachoongozwa na Muungano wa Ulaya, EU (EUFOR ALTHEA) kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Akihutubia Baraza la Usalama kabla ya kura ya azimio hilo, Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa wa ngazi ya juu nchini Bosnia na Herzegovina, Valentin Inzko, amesema nchi hiyo inapokaribia kuadhimisha miaka ishirini tangu mikataba ya amani iliposainiwa tarehe 21 Novemba 1995 na kumaliza mzozo mbaya zaidi wa Ulaya tangu vita vikuu vya pili vya dunia kumalizika, ni wakati mwafaka wa kutafakari kuhusu mafanikio yaliyopatikana, na mambo yaliyosalia kufanywa.

Amesema mengi ya mafanikio ya nchi hiyo yalipatikana katika miaka kumi ya kwanza baada ya kumalizika vita.

“Uhuru wa kutembea uliwekwa, wakimbizi milioni moja walirejea nyumbani baada ya mzozo, serikali ya kitaifa iliwekwa, uchumi ukaimarishwa na mfumo wa sheria ukawekwa. Vikosi vitatu vya jeshi na mawaziri watatu wa Ulinzi waliokuwa wamepigana waliletwa pamoja chini ya Wizara moja ya Ulinzi.”

Hata hivyo, amesema katika miaka kumi iliyopita, nchi hiyo haijakuwa ikielekea kwenye mkondo upasao, na matokeo yake imekuwa na masikitiko kwa jamii ya kimataifa na raia wa nchi hiyo kuvunjwa moyo.

Tunapoingia muongo wa tatu wa mchakato wa amani, tunapaswa kuwa na matarajio zaidi, ili tuone matokeo ya dhati na kasi inayotia moyo. Naamini kuwa maendeleo makubwa yanaweza kupatikana katika miaka kumi ijayo, iwapo mambo mawili ya msingi yatafanyika: utashi wa kisiasa wa kufanya marekebisho makuu ili kuisongesha nchi mbele. Pili, utashi usiolegea wa kuheshimu mikataba ya amani.”