OCHA yasifu harakati za wanawake Mali kukwamua nchi yao

OCHA yasifu harakati za wanawake Mali kukwamua nchi yao

Mkuu wa operesheni kwenye ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uratibu wa misaada ya kibinadamu, OCHA, John Ging, amepongeza harakati za wanawake katika kukwamua Mali kutoka janga la mzozo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini New York, Marekani baada ya ziara yake ya siku tatu nchini humo, Bwana Ging amesema ameshuhudia ujasiri na ari ya wanawake katika kuhakikisha wanachangia katika uchumi wa nchi yao.

Amesema miaka miwili iiyopita wanawake walihaha kuongoza jamii zao katikati ya janga la vita lakini sasa wanamiliki biashara zinazochangia uchumi.

(Sauti ya Ging)

“Nilitembelea  miradi kadhaa ambayo ilikuwa ni kampuni ndogo zinazoajiri wanawake na zinaongozwa na  wanawake. Ari na matokeo yatokanayo na miradi hiyo yalikuwa yanatia moyo sana.”

Halikadhalika Bwana Ging amesifu busara inayoonyeshwa na pande husika kwenye mzozo nchini Mali kwa kufikia makubaliano mwezi Juni mwaka huu.

Amesema makubaliano hayo ni fursa ya kujenga amani ya kudumu na hivyo ni lazima iungwe mkono kupitia usaidizi wa kifedha na kibinadamu kwa maendeleo ya Mali.