Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ziara Saudia, Ban akutana na waziri wa Brazil

Ziara Saudia, Ban akutana na waziri wa Brazil

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aliyeko ziarani  huko Saudi Arabia amekuwa na mazungumzo na Waziri wa mambo ya nje wa Brazil, Mauro Vieira mjini Riyadh.

Katika mazungumzo hayo, Bwana Ban ameshukuru serikali ya Brazil kwa usaidizi wake wa dhati kwenye kupitisha ajenda ya maendeleo endelevu, SDG ijulikanayo pia kama ajenda 2030 na kueleza kuwa ni matumaini yake malengo hayo yatatekelezwa ipasavyo na nchi wanachama.

Halikadhalika wawili hao wamejadili mkutano ujao wa 21 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi utakaofanyika Paris, Ufaransa.

Ban amesema ni matumaini yake kuwa Brazil itaendelea kutekeleza dhima muhimu kuelekea mkutano huo sambamba na ushiriki wake.

Katika Mkuu amegusia pia operesheni za ulinzi wa amani akitoa shukrani zake kwa Brazil huko Haiti kupitia ujumbe wa ulinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa MINUSTAH na usaidizi wake wa maendeleo ya nchi hiyo.

Masuala mengine waliojadili Bwana Ban na Waziri Vieira ni mchakato wa amani Colombia, Mashariki ya Kati, Syria na uhusiano kati ya Israel na Palestina.