Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yakaribisha uamuzi wa Canada kuhifadhi maelfu ya wakimbizi

UNHCR yakaribisha uamuzi wa Canada kuhifadhi maelfu ya wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, limekaribisha tangazo la serikali ya Canada la kuchukua idadi ya wakimbizi 25,000 kutoka Syria, ifikapo mwaka 2015 kupitia programu ya kibinadamu ya uandikishaji wa wakimbizi.

Taarifa ya UNHCR inasema kuwa hatua hiyo ni ukarimu mkubwa wa mshikamano na watu wa Syria na mataifa jirani na nchi hiyo, ambazo kwa pamoja zinahifadhi wakimbizi zaidi ya milioni nne na kuwa sehemu ya adha ya mgogoro.

Kamishana mkuu wa UNHCR António Guterres ameyataka mataifa mengine kuiga mfano wa Canada kwa jinsi ambavyo wanatumia rasilimali zao kwa kuongeza hifadhi kwa wakimbizi wa Syria  ambao wanaweza kujenga maisha yao katika nchi salama bila kufanya safari hatarishi.

Kamishna Guterres ameihakikishia Canada kuwa UNHCR itafanya kazi na nchi hiyo hususani katika mamlaka ya uhamiaji ili kuruhusu utambulisho wa haraka wa Wasyria walioko hatarini huko Mashariki ya Kati hususani Lebanon na Jordan,  na hatimaye kuwawezesha kuhamia Canada ambapo watapata vibali vya uraia vya muda na kuwaruhusu kisheria kuomba uraia baada ya miaka minne.