Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vyakula vya jamii ya kunde vyachangia lishe bora na uhakika wa chakula

Vyakula vya jamii ya kunde vyachangia lishe bora na uhakika wa chakula

Shirika la Chakula na Kilimo duniani FAO limesema vyakula vyote vya jamii ya kunde ni nafuu na vitamu vikiwa na kiwango kikubwa cha protini na hivyo kuweza kutumiwa badala ya nyama. Taarifa zaidi na Grace Kaneyia.

(Taarifa ya Grace)

FAO imetoa kauli hiyo leo ikizindua mwaka wa kimataifa wa vyakula jamii ya kunde, ili kumulika manufaa ya vyakula hivyo ambavyo ni pamoja na maharage, choroko, dengu na aina zote za kunde ambazo ni lishe bora, vitamin nyingi, mafuta kidogo na bei nafuu ikilinganishwa na nyama.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, mkurugenzi mkuu wa FAO Jose Graziano Da Silva amesema jamii za kunde inaweza kuchangia katika kupambana na njaa katika nchi zinazoendelea.

(Sauti Ya Bwana Da Silva)

“ Vyakula jamii ya kunde vinakuwa na asilimia hadi 25 ya protini. Ni muhimu kwa uhakika wa chakula kwa idadi kubwa ya watu, hasa Amerika ya Kati na Kusini, sisi ni walaji wa maharage. Lakini pia Afrika na Asia ambapo ni chakula asili kinacholimwa na wakulima wadogo wadogo”

Aidha FAO imesema kilimo cha jamii ya kunde huchangia kulinda uhai wa ardhi na kuimarisha kipato cha wakulima.