Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto zaidi Guinea kunufaika kwa lishe shuleni mwaka huu

Watoto zaidi Guinea kunufaika kwa lishe shuleni mwaka huu

Zaidi ya watoto 240,000 watapokea chakula shuleni mwaka huu nchini Guinea, kufuatia Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP kupanua mpango wake wa chakula shuleni kutoka shule 735 za msingi hadi shule 1,605 nchini humo.

WFP imesema inarejelea mpango wake wa kutoa chakula shuleni katika maeneo manne ya nchi, muhula na mwaka mpya wa shule unapoanza wiki hii.

Ikishirikiana na Wizara ya Elimu nchini Guinea na wadau wengine, WFP itatekeleza mpango huo wa kutoa chakula kila siku kwa watoto katika maeneo yasiyo na uhakika wa chakula nchini, na ambayo yameathiriwa zaidi na umasikini na utapiamlo.

Kufuatia mlipuko wa Ebola, shule za umma nchini Guinea ziliendelea kufungua baada ya mapumziko wa majira ya joto kali mwaka 2014, ili kudhibiti kuenea kwa kirusi cha Ebola, lakini zilianza tena kufunguliwa mnamo mwezi Januari mwaka huu.