Hali Burundi tete, mauaji holela yaongezeka- Kamishna Zeid

9 Novemba 2015

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu, Zeid Ra’ad Al-Hussein, amesema hali ya haki za binadamu nchini Burundi imezorota zaidi katika siku chache zilizopita, akiongeza kuwa mbali na mauaji yanayoongezeka, kuna dalili za hatari ya hali kuwa mbaya zaidi, na madhara yake kuenea kikanda.

Kamishna Zeid amesema hayo akilihutubia Baraza la Usalama kwa njia ya video kutoka Geneva, akionya kuwa Burundi imefikia kwenye ncha ya machafuko, na kwamba anaamini nchi wanachama na Baraza la Usalama linaweza kuingilia kati ili kuzuia kurudiwa kwa maafa ya zamani.

Kamishna Zeid amesema ofisi yake imerekodi idadi ya mauaji inayoongezeka nchini Burundi, hususan mjini Bujumbura, yakiwemo mauaji mengi yanayodaiwa kuwa kwa misingi ya kisiasa.

(Sauti ya Bwana Zeid)

“Angalau watu 240 wameuawa tangu maandamano ya Aprili, miili ikitupwa mitaani takribani kila usiku. Kumekuwa na visa vya mamia ya kuwakamata na kuwazuilia watu kiholela katika mwezi uliopita pekee, kukiwalenga wapinzani, wanahabari, watetezi wa haki za binadamu na familia zao, watu wanaohudhuria matanga ya waliouawa, na wakazi wa maeneo yanayodhaniwa kuunga mkono upinzani.”

Kamishna Zeid amesema ingawa kuingilia kati kwa ofisi yake kulisababisha kuachiliwa kwa watu 340 waliokuwa kizuizini mwezi uliopita, bado watu wanaotoa maoni ya kupinga serikali wanaishi kwa mazingira ya uoga mkubwa.

(Sauti ya Bwana Zeid)

“Kutekwa na kuuawa kwa Willy Nzitonda, mwanawe mtetezi wa haki za binadamu, Pierre-Claver Mbonimpa mwenye umri wa miaka 25, ni mfano mmoja wa hivi karibuni zaidi unaotia uchungu. Bwana Mbonimpa mwenyewe alijeruhiwa vibaya wakati wa jaribio la kumuua mnamo mwezi Agosti, na mwana mkwewe ambaye pia ni mtetezi wa haki za binadamu, aliuawa mwezi uliopita.”

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter