Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Somalia hatarini kukumbwa na mafuriko – OCHA

Somalia hatarini kukumbwa na mafuriko – OCHA

Zaidi ya watu 90,000 wameathirika kwa mvua kubwa na mafuriko yanayokumba Somalia tangu mwisho wa mwezi Oktoba, imesema Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu, OCHA.

OCHA imesema ni watu karibu 43,000 ambao wamelazimika kuhama makwao na wengine wako hatarini kuondoka kwenye makazi yao huko kusini mwa nchi.

Mashirika ya kibinadamu tayari yameanza kusambaza misaada iliyokuwa imehifadhiwa kwa ajili ya mahitaji ya dharura kama vile vifaa vya kujisafi na vya kusafishia maji ya kunywa.

Aidha OCHA imeongeza kwamba visa vya kipindupindu vimeripotiwa kwenye maeneo ya Jowhar, Kismayo na Mogadishu, ikihofia kwamba idadi itaongezeka kwa sababu ya kuendelea kwa mafuriko.

Vifaa vya matibabu na vifurushi vya chakula vimekusanywa kwa ajili ya mahitaji yatakayoibuka iwapo hali itazidi kuwa mbaya.