Ban Ki-moon alaani mauaji ya mfanyakazi wa Umoja wa Mataifa Burundi

9 Novemba 2015

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amelaani vikali mauaji ya watu wapatao Saba yaliyotokea kwenye baa moja huko Kanyosha, mjini Bujumbura nchini Burundi siku ya jumamosi.

Miongoni mwa wahanga ni mfanyakazi wa Umoja wa Mataifa.

Kwenye taarifa yake iliyotolewa leo na msemaji wake, Katibu Mkuu amesema watekelezaji wa uhalifu huo wanadaiwa kuwa watu waliovaa nguo za polisi.

Katibu Mkuu amekariri wito wake wa kusitisha ghasia na mauaji nchini humo, akiisihi serikali kuanzisha uchunguzi thabiti kuhusu mauaji hayo na kupeleka watekelezaji mbele ya sheria.

Amesisitiza kwamba serikali inawajibika kuhakikishia usalama wa raia wake na wa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa nchini humo.

Aidha bwana Ban amesikitishwa na ripoti zilizotokea leo za mauaji yaliyoripotiwa kufanywa wakati zoezi la kutaka watu kusalimisha silaha kwa nguvu likiendelea mjini Bujumbura.

Amevisihi vikosi vya usalama kujizuia kutumia ghasia itakayoweza kuibua mvutano zaidi nchini humo.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter