Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kamisheni ya Ulaya imetukwamua:UNRWA

Kamisheni ya Ulaya imetukwamua:UNRWA

Kamisheni ya Ulaya imetoa kiasi cha dola milioni 2.7 ili kusaidia wakimbizi wa kipalestina walioko chini Syria kiasi hicho kikiwa kinafanya mchango wa kamisheni hiyo kwa mwaka huu uwe dola milioni 5.6.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Palestina UNRWA katika taarifa yake linasema mchango huo umekuja wakati huu ambapo hali ya kibinadamu inazorota nchini Syria na kuongeza kuwa msaada huo utatumika katika mpango wa dharura wa usaidizi, unaowalenga wakimbizi zaidi ya laki nne katika kuwapatia mahitaji muhimu.

Mkurugenzi wa Masuala ya UNRWA nchini Syria Michael Kingsley-Nyinah amesema wakimbizi wa kipalestina wanaendelea kuteseka na hivyo msaada huo wa kamisheni ya Ulaya utawezesha kuwafikia wakimbizi wengi zaidi kwa misaada ya uokozi.

Shirika hilo limesema kuwa kadhalika msaada huo utasaidia katika mpango wa shirika wa kusaidia wakimbizi wakati wa majira ya baridi kali ikiwa wakimbizi wa kipalestina wanajiandaa kukabiliana na awamu ya tano ya majira ya baridi kali wakiwa katika machafuko.