Kutoka UNSOA kwenda UNSOS kuimarisha utendaji Somalia
Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa leo limepitisha kwa kauli moja azimio la kubadili majukumu ya ofisi yake ya usaidizi wa operesheni wa kikosi cha Muungano wa Afrika huko Somalia, AMISOM kutoka UNSOA kwenda UNSOS. Taarifa zaidi na Amina Hassan.
(Taarifa ya Amina)
Azimio hilo limepitishwa katika kikao cha ngazi ya mawaziri, na limezingatia tathmini ya AMISOM iliyofanywa na Muungano wa Afrika na Umoja wa Mataifa ikitaka kwanza ofisi hiyo ibebe jina linaloakisi majukumu yake kwa Somalia yote.
Kupitia azimio hilo, UNSOS sasa itasaidia AMISOM, jeshi la kitaifa la Somalia na ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, UNSOM ambapo mwakilishi wa katibu Mkuu nchini Somalia Nicholas Kay amesema limekuja wakati muafaka wakati nchi hiyo inajizatiti kusonga mbele na kwamba...
(Sauti ya Kay)
“Sitachoka kusema kuwa Somalia sasa inakabiliwa na matatizo ya nchi inayohaha kujinasua badala ya kusambaratika.”
Waziri Mkuu wa Somalia, Omar Abdirashid Ali Sharmake amekaribisha azimio hilo huku akihakikisha wajumbe utayari wa wa serikali kuu na majimbo katika kusongesha maslahi ya wananchi akisema..
(Sauti ya Sharmake)
“Sote tunatambua kuwa ni kwa maslahi ya Somalia kukamilisha michakato ya ujenzi wa nchi na uchaguzi ndani ya awamu ya serikali ya sasa inayomaliza muda wake Agosti 2016.”
Wakati huo huo, Baraza la Usalama baadaye leo litakuwa na kikao kuhusu Burundi wakati huu ambapo mauaji ya raia yamekuwa yakiripotiwa kila uchao.