Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ICC iheshimu uamuzi wa Baraza Kuu la mkataba wa Roma:Macharia

ICC iheshimu uamuzi wa Baraza Kuu la mkataba wa Roma:Macharia

Kenya imeitaka mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC kuzingatia makubaliano yanayopitishwa na vikao vya nchi wanachama wa mkataba wa Roma ulioanzisha mahakama hiyo.

Hiyo ni kwa mujibu wa mwakilishi wa kudumu wa Kenya kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Macharia Kamau wakati akihutubia Baraza Kuu baada ya kuwasilishwa kwa ripoti ya utendaji ya ICC.

Balozi Kamau ametolea mfano kuwa mkutano wa Baraza la nchi wanachama wa mkataba wa Roma ulifanyia marekebisho Ibara ya 68 ya mkataba huo, marekebisho ambayo yalitaka kutotumika kwenye kesi yoyote mbele ya mahakama hiyo ushahidi wowote uliokuwa umerekodiwa kabla ya mabadiliko hayo.

Hata hivyo amesema amesema hata kabla mwaka mmoja kupita, ICC ilikiuka utashi wa mkutano huo na kutumia ushahidi wa aina hiyo kwenye kesi kuhusu Kenya.

(Sauti ya Balozi Kamau)

"Cha kusikitisha ni kwamba mahakama imekwenda mbali zaidi na kukubali matumizi ya ibara ya 68, hiyo sio tu kwamba inakiuka mabadiliko ya kanuni za matumizi ya sheria hiyo lakini inafanya hivyo huku ikielewa kabisa makubaliano hayo yaliyofikiwa Novemba 2013."

Mwakilishi huyo wa kudumu wa Kenya amesema ni vyema ikumbukwe kuwa matumizi ya shuhuda zilizorekodiwa kabla ya mabadiliko ya sheria haikidhi viwango vyovyote vya kisheria katika mahakama ya nchi yoyote ile hata zile za viwango vya chini.