Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kamishna Zeid alaani mauaji ya mtoto wa mwanaharakati Mbonimpa Burundi

Kamishna Zeid alaani mauaji ya mtoto wa mwanaharakati Mbonimpa Burundi

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa, Zeid Ra’ad Al Hussein, amelaani vikali mauaji ya Welly Nzitonda, mwanae Pierre Claver Mbonimpa, ambaye ni mtetezi maarufu zaidi wa haki za Binadamu nchini Burundi.

Marehemu aliripotiwa kukamatwa na polisi saa tano asubuhi, na mwili wake ukapatikana mchana katika mtaa wa Mutakura.

Kijana huyo aliyeuawa mapema leo ni mtu wa pili katika familia ya Mbonimpa kuuawa katika kipindi cha wiki chache, mwana mkwe wake akiwa ameuawa mnamo tarehe tisa Oktoba, 2015.

Bwana Pierre Claver Mbonimpa mwenyewe alinusurika kuuawa mwezi Agosti mwaka huu 2015, na bado anapokea matibabu ng’ambo.

Kamishna Zeid amesema mauaji hayo yanathibitisha hofu kuwa kuna sera ya kimfumo ya kuwalenga wapinzani, wanahabari, watetezi wa haki za binadamu na raia wa kawaida wanaodhaniwa kuipinga serikali. Ameongeza kuwa hadi sasa kumekuwa na ukwepaji sheria kwa uhalifu huo wote.