Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sanaa za wakimbizi zabadilisha mtazamo wa jamii nchini Kenya

Sanaa za wakimbizi zabadilisha mtazamo wa jamii nchini Kenya

Leo ni siku ya mwisho ya maonyesho ya sanaa zinazoandaliwa na wakimbizi huko mjini Nairobi nchini Kenya kupitia mradi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR, huku tayari mafanikio yakipatikana. Taarifa zaidi na Priscilla Lecomte.

(Taarifa ya Priscilla)

Mwakilishi wa UNHCR nchini Kenya Raouf Mazou ameiambia idhaa hii kwamba tayari kazi nyingi za sanaa zimeuzwa na mradi huo umeonyesha uwezekano wa kusaidia wakimbizi kujitegemea kupitia njia zisizo za kawaida.

Aidha amesema kupitia mradi huo wakimbizi wameweza kujiamini lakini pia mtazamo wa jamii kuhusu wakimbizi hawa umeanza kubadilika, kupitia ushirikiano na wasanii maarufu Octopizzo na Victor Ndula, akisema:

(Sauti ya bwana Mazou)

“Sawa, ni watu ambao wametafuta hifadhi kwa sababu ya mazingira kwenye nchi yao, lakini hakuna sababu ya kuwabagua, Ni ujumbe unaopitishwa kila mara na Octopizzo na Victor Ndula, na sisi tunaona ni kitu kizuri sana na tunadhani kitabadilisha mitazamo ya watu hapa Kenya kuhusu wakimbizi, baadhi ya watu lakini, siyo wote, tusichukue vitu kijumla jumla”

Amesisitiza kwamba Kenya ni nchi ya pili barani Afrika kwa kupokea wakimbizi na hilo ni sadaka kubwa, wengi wa wakimbizi kutoka Sudan Kusini na Somalia wakiwa wameishi kambini tangu miaka ya tisini.