Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Adhabu ya kifo si muarobaini wa uhalifu: Ban

Adhabu ya kifo si muarobaini wa uhalifu: Ban

Kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa kumefanyika uzinduzi wa kitabu kuhusu kuondokana na adhabu ya kifo ambapo Katibu Mkuu Ban Ki-moon amesema ni fursa nyingine ya kushawishi nchi zaidi kutupilia mbali adhabu hiyo.

Ban amesema pamoja na kwamba adhabu hiyo ni ukiukaji wa haki za binadamu, kumekuwepo pia na adhabu za kifo zinazotolewa kimakosa akisema hata kwa kufanya hivyo serikali zinakuwa zimekosesha zaidi watu haki zao.

Amesema hadi sasa hakuna mtu aliyethibitisha kuwa adhabu ya kifo inapunguza uhalifu na ukweli unaouma ni kwamba adhabu hiyo ni baguzi.

Katibu Mkuu amesema ni baguzi kwa kuwa tafiti zimebaini kuwa iwapo mtu ni maskini, anatoka jamii ndogo au mlemavu wa akili yuko hatarini zaidi kuhukumiwa adhabu hiyo awe ana makosa au la.

Ban amesema lazima harakati za kutokomeza adhabu hiyo ziendelee kwani licha ya baadhi ya nchi kuondokana nayo, nyingine zimeirejesha.

Tukio hilo lilihudhuriwa pia na mmarekani Kirk Bloodsworth ambaye alihukumiwa adhabu ya kifo lakini kipimo cha vijinasaba kilibainisha kuwa si yeye ambaye alitenda kosa.