Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wawakilishi wa Libya msizuie mchakato wa demokrasia- Leon

Wawakilishi wa Libya msizuie mchakato wa demokrasia- Leon

Mwakilishi wa Katibu Mkuu na Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, UNSMIL, Bernardino Leon, ametoa wito kwa viongozi wa bunge la jumla na bunge la Congress nchini Libya kusikiliza wito ndani ya mabunge yao na wa watu wa Libya, na kujiepusha na vitendo vyovyote vya kuzuia au kuvuruga mchakato wa demokrasia na kudunisha ufanisi wa mchakato wa mazungumzo ya kisiasa.

Bwana Leon amesema hayo wakati akilihutubia Baraza la Usalama, ambalo limekutana leo kujadili kuhusu hali nchini Libya.

Bwana Leon amesema viongozi wa Libya wana fursa ya aina yake ya kufikia makubaliano ya kisiasa yatakayoiepusha nchi yao na watu wao umwagaji damu na uharibifu zaidi.

Kwa mantiki hiyo, amesema kuwa makubaliano ya kisiasa yaliyofikiwa katika mkakati na mchakato wa mazungumzo, yametokana na mwaka mzima wa mazungumzo tatanishi na ulegezaji misimamo ambao ulilenga kuweka msimamo wa kati unaowakutanisha Walibya wote .

“Mkataba uliopendekezwa haujanuia kuwa suluhu matatizo yote ya Libya, lakini ni kwa minajili ya kuweka fungu la utaratibu na kanuni zinazoweza kuongoza awamu itakayofuata ya mpito wa kisiasa nchini Libya, hadi pale mchakato wa kuunda katiba utakapomalizika."

Kwa mantiki hiyo Bwana Leon ametoa wito kwa viongozi wa Libya kuzingatia maslahi ya taifa lao na kulinda umoja wa nchi, uhuru na mipaka yao.