Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNESCO yaridhia Mpango kazi wa elimu hadi 2030

UNESCO yaridhia Mpango kazi wa elimu hadi 2030

Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu Sayansi na Utamaduni UNESCO limezindua mpango kazi wa elimu hadi mwaka 2030.

Tukio hilo limefanyika jumatano wakati mkutano mkuu wa UNESCO ukiendelea mjini Paris Ufaransa.

Mpango kazi huo umetaja kanuni nne muhimu: elimu bora inapaswa kuwa bure na lazima kwa wote, elimu ni wajibu wa umma, watu wazima wanapaswa kupewa fursa ya kujisomea maishani mwao yote, na usawa wa kijinsia unapaswa kupewa kipaumbele.

Akizungumza wakati wa tukio hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa UNESCO Bi Irina Bokova amekariri umuhimu kwa serikali kuwekeza asilimia 6 ya pato la taifa kwa elimu, huku akisisitiza kwamba ili kufikia hilo lazima nchi zilizoendelea zitimize ahadi zao za kuchangia asilimia 0.7 ya kipato chao kwa usaidizi wa maendeleo.