Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Beckham ashiriki kampeni ya kupambana na utapiamlo Papua New Guinea

Beckham ashiriki kampeni ya kupambana na utapiamlo Papua New Guinea

Balozi Mwema wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF David Beckham amekutana leo na watoto wanaopatiwa tiba dhidi ya utapiamlo nchini Papua New Guinea kwenye hospitali iliyofadhiliwa na shirika hilo.

Hii ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na UNICEF ikisema kwamba mtoto mmoja kati ya 13 nchini humo hufariki dunia kabla ya kufikia umri wa miaka 5, utapiamlo ukiwa ni sababu ya kwanza.

Aidha UNICEF imesema karibu nusu ya watoto nchini Papua New Guinea wamedumaa.

Beckham ambaye amezindua awali mwaka huu mfuko wake wa ufadhili uitwao 7: The David Beckham UNICEF Fund, ameeleza kufuraishwa na kuona matumizi ya fedha hizo katika kuimarisha maisha ya watoto duniani kote mathalani kwenye hospitali aliyoitembelea.

Halikadhalika, Bwana Beckham pamoja na wachezaji wastaafu wengine kama vile Zinedine Zidane tarehe 14 mwezi huu watacheza mechi ya uchangishaji fedha kwa ajili ya watoto, ambapo faida yake itanufaisha mfuko wake wa UNICEF.