Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban ahimiza mashauriano ya dhati kuhusu Sahara Magharibi

Ban ahimiza mashauriano ya dhati kuhusu Sahara Magharibi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesema wakati mvutano kuhusu mustakhbali wa Sahara Magharibi na mateso uliozua kwa wanadamu ukiingia mwaka wa 40, hali kaskazini magharibi mwa Afrika inaendelea kusikitisha.

Ban amesema mgogoro huo ni lazima ukomeshwe ili watu wa ukanda huo waweze kukabiliana na changamoto zao za pamoja na kutimiza uwezo wao.

Katibu Mkuu amesema hatma ya eneo hilo inaendelea kujadiliwa katika mchakato unaosimamiwa na ofisi yake kulingana na maazimio ya Baraza la Usalama. Ban ameeleza kusikitishwa kwamba mapendekezo ya Aprili 2007 ya Ufalme wa Morocco na Polisario Front hayajfungua njia ya mashauriano ya dhati ambayo yeye na Baraza la Usalama wametolea wito mara kwa mara.

Kwa mantiki hiyo, ametoa wito kwa wote wanaohusika katika eneo hilo na katika jamii ya kimataifa kwa ujumla, kuunga mkono juhudi za Mjumbe wake Christopher Ross za kuwezesha kuzindua mashauriano ya dhati katika miezi ijayo.