Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lajadili Libya, Bensouda ahutubia

Baraza la Usalama lajadili Libya, Bensouda ahutubia

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo limekuwa na kikao kuhusu hali nchini Libya, ambapo limesikiliza pia hotuba ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC, Fatou Bensouda. Taarifa kamili na Grace Kaneiya.

(Taarifa ya Grace)

Katika hotuba yake, Bi Bensouda amesema machafuko nchini Libya yamesababisha kusambaratika kwa taasisi za kitaifa na utawala wa sheria, na hivyo kuweka mazingira ya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na sheria ya kimataifa ya kibinadamu.

Bi Bensouda amekariri wito wake wa awali kwa jamii ya kimataifa kuisaidia Libya kuimarisha uwezo wake kitaifa kukabiliana na uhalifu unaotajwa katika Mkataba wa Roma, kupitia kuweka kikundi cha kimataifa kinachohusika na masuala ya sheria.

Amesema mafanikio ya hivi karibuni kuelekea kuweka serikali ya umoja wa kitaifa nchini Libya, yanaweza kuongeza matumaini ya kuanzisha tena mazungumzo kuhusu pendekezo hilo la kikundi cha kimataifa kuhusu masuala ya sheria.

Ametoa wito kwa nchi zote ambazo hazijatoa ushirikiano na ofisi yake kufanya hivyo, akitoa sababu:

“Baadhi ya ushahidi na watu wanaohitajika na ofisi yangu wapo nje ya Libya, na wanaweza tu kufikiwa kupitia kwa ushirikiano wa nchi husika. Kumaliza ukwepaji sheria kwa uhalifu mbaya zaidi nchini Libya ni lengo muhimu, ambalo linaweza kutimizwa na linalohitajika kwa amani endelevu na utulivu nchini humo.”