Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yazindua changisho jipya kwa wakimbizi Ulaya

UNHCR yazindua changisho jipya kwa wakimbizi Ulaya

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, limezindua leo changisho jipya la dola milioni 96 za ziada kusaidia Ugiriki na nchi zingine Mashariki mwa Ulaya kutoa usaidizi kwa wakimbizi na wahamiaji wanaowasili Ulaya kupitia Bahari ya Mediterenia. Taarifa kamili na Priscilla Lecomte.

(Taarifa ya Priscilla)

UNHCR imesema kuwa majira ya baridi kali katika ukanda huo huenda yakaongeza taabu ya maelfu ya wakimbizi na wahamiaji wanaowasili Ugiriki na kusafiri kupitia nchi za eneo la Balkan, na yanaweza pia kusababisha vifo iwapo hatua zifaazo hazitachukuliwa kwa dharura.

Mpango mpya wa UNHCR wa majira ya baridi kali unatakadiria kuwa huenda wakimbizi na wahamiaji wapya 5,000 wakawasili kila siku kutoka Uturuki kati ya mwezi Novemba na Februari mwakani.

Mpango huo unazingatia kuweka mikakati ya kusaidia nchi zilizoathiriwa mathalan Croatia, Ugiriki, Serbia, Slovenia na Macedonia ilokuwa sehemu ya Jamhuri ya Yugoslavia kwa kuandaa na kuboresha makazi yaliyopo kukabiliana na majira ya baridi kali.