Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchini Yemen kimbunga Chapala chaleta maangamizo

Nchini Yemen kimbunga Chapala chaleta maangamizo

Kimbunga Chapala kimebainiwa kuwa dhoruba ya tropiki tu na watalaam wa utabiri wa hali ya hewa, na nguvu yake inatarajiwa kupungua tena katika kipindi cha saa 12.

Hii ni kwa mujibu wa ofisi ya Umoja ya Mataifa la Kuratibu Misaada ya Kibinadamu OCHA ambayo imesema leo kwamba hata hivyo tayari baadhi ya maeneo yameathiriwa na mvua kubwa kikiwemo kisiwa cha Socotra ambapo nyumba 400 zimeharibiwa.

Akizungumza na redio ya Umoja wa Mataifa, mratibu wa maswala ya kibinadamu nchini Yemen Johannes van der Klaauw amesema lwamba OCHA inakadiria kuwa watu milioni 1.8 wataathirika na kimbunga hicho.

(Sauti ya Bwana van der Klaauw)

“ Tayari tumekadiria kwamba watu zaidi ya 40,000 wamekimbia makwao kwa sababu ya kimbunga na watu hawa hawawezi kurudi makwao kwa sababu nyumba zao zimepelekwa na dhoruba na hawana tena ardhi ya kulima au boti za kuvua.”

Tayari Shirika la Afya duniani WHO limepatia hospitali nane lita 20,000 za mafuta huku vifaa vingine viko njiani.

Aidha Mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa yametuma misafara ya misaada ya kibinadamu ikiwa ma shehena za mahema na vifaa vya kujisafi na kupikia.