Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Elimu yaweza kujenga mitazamo ya kupambana na rushwa - Fedotov

Elimu yaweza kujenga mitazamo ya kupambana na rushwa - Fedotov

Mkutano wa Sita wa nchi wanachama wa mkataba wa kimataifa dhidi ya rushwa, umeingia siku ya tatu hii leo mjini St. Petersburg, Urusi ambapo, huku elimu ikitajwa kuwa yenye umuhimu mkubwa katika kujenga mitazamo inayohitajika katika kupambana na rushwa.

Kwenye kikao kuhusu kupinga rushwa kupitia kwa elimu, Mkurugenzi Mtendaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya na Rushwa, Yury Fedotov, amesema kuwa kuchagiza akili za viongozi na wasomi wa vizazi vijavyo ni sehemu ya mchakato wa kutumia elimu kupambana na rushwa.

Bwana Fedotov amesema, kushirikisha wasomi kunaweza kuimarisha juhudi za kutekeleza ipasavyo mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya rushwa.

“Hicho ndicho UNODC inalenga kutimiza kwa mkakati wa elimu ya kupinga rushwa. Tunaunga mkono juhudi za kuunganisha elimu ya kupinga rushwa na kozi za vyuo vikuu na taasisi zingine katika programu za elimu. Mbinu hii imetokana na misingi kuwa, hatua kama hiyo inaweza kutekelezwa, inasaidia na ni bure kwa matumizi ya wote.”