Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM wataka wahudumu wa kibinadamu waliotekwa Lybia waachiwe huru mara moja

UM wataka wahudumu wa kibinadamu waliotekwa Lybia waachiwe huru mara moja

Mratibu wa Umoja wa Kimataifa wa masuala ya kibinadamu nchini Libya, Ali Al-Za’tari, amelaani kuendelea kutekwa kwa wahudumu wawili wa kibinadamu Kusini mwa nchi hiyo na kutoa wito waachiliwe huru mara moja bila masharti yoyote.

Bwana Al-Za’tari ameonya kuwa uwezo wa kufikisha misaada muhimu kwa wenye uhitaji Kusini mwa Libya unaathiriwa na vitisho kwa wahudumu wa kibinadamu.

Aidha, ameeleza wasiwasi wake kuhusu mazingira mabaya wanamozuiliwa wahudumu hao waliotekwa tangu tarehe 5 Juni, 2015 kule al-Shwayrif kusini mwa Libya, wakiwa njiani kupeleka misaada kusini magharibi mwa nchi.

Wahudumu hao wawili, Bwana Mohamed al-Monsef Ali al-Sha’lali na Bwana Walid Ramadan Salhub, ni wafanyakazi wa shirika la kibinadamu la Tahir Azzawy, ambalo husaidia mashirika kadhaa ya kimataifa katika kutekeleza majukumu yao.