Skip to main content

Kimbunga Chapala chatikisa Yemen

Kimbunga Chapala chatikisa Yemen

Mashirika ya umoja wa mataifa yamejikita katika kuandaa mikakati  ya kuisaidia Yemen kukabiliana na kimbunga Chapala huku hofu ikiwa imetanda kuwa mvua kubwa yaweza kunyesha na kuleta uharibifu mkubwa wakati huu ambapo wananchi wanakabiliwa na mapigano nchini mwao.Taarifa zaidi na  John Kibego.

(Taarifa ya Kibego)

Shirika la Hali ya Hewa Ulimwenguni (WMO) limesema, lina hofu kuwa kimbunga hicho kinaambatana na dhoruba kali ilihali Wayemen hawajazoea hali hiyo na pia taifa halina miundombinu ya kudhibiti athari zake.

Tayari Kimbunga Chapala kimesababisha upepo  unaovuma kwa kilometa 145 kwa saa sambamba na mvua .

Shirika la Afya Duniani limekuwa likisambaza vifaa vya kudhibiti kiwewe miongoni mwa raia pamoja na mafuta hospitalini na magari ya kusafirisha wagonjwa, huku  maporomoko ya ardhi yakitarajiwa.

Clare Nullis ni Afisa kutoka WMO.

(Sauti ya Clare)

"Tunatarajia athari kuendelea, kwa sababu hofu yetu kubwa kuhusu kimbunga hiki ni uwezekano wa mvua kubwa.Cha kusisitiza hapa ni kwamba, Yemen ni eneo kame sana, na haina miundombinu ya kukabiliana na hali hii, na hivyo tunategemea kimbunga hiki kitakuwa na athari mbaya sana. "

Ofisi ya Umoja wa Matafa ya Kuratibu misaada ya dharura (OCHA) inaonya kuwa kimbuga kicho kitaathiri zaidi maeneo ya Shabwah na Hadhramaut, yenye takriban watu mil;ioni 1.8.