Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano kuhusu rushwa wamulika biashara haramu ya viumbe vya pori

Mkutano kuhusu rushwa wamulika biashara haramu ya viumbe vya pori

Mkutano wa Sita wa nchi wanachama wa mkataba wa kimataifa dhidi ya rushwa, unaendelea huko St. Petersburg nchini Urusi ambapo leo washiriki wamemulika uhusiano baina ya rushwa na aina tofauti za uhalifu wa kupangwa unaovuka mipaka, ukiwemo biashara haramu ya wanyamapori na misitu.

Katika mahojiano na Redio ya Umoja wa Mataifa, Mkurugenzi Mtendaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya na Uhalifu, Yury Fedotov, amesema mkutano wa leo umetoa fursa mwafaka ya kujadili jinsi utekelezaji wa mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu rushwa unavyoweza kusaidia juhudi za kupambana na uhalifu unaohusu wanyamapori na misitu.

"Kwa hiyo mkutano huu umekuwa muhimu sana katika kuongeza uelewa na kuelekeza juhudi katika maeneo tofauti ambapo tunaweza kusaidia kukabiliana na rushwa, pamoja na uhalifu unaohusu wanyamapori na misitu.”

Mkutano huo unafuatia azimio la Baraza Kuu lililopitishwa mapema mwaka huu, likitaja umihumu wa kutekeleza siyo tu Mkataba wa Kimataifa kuhusu biashara katika viumbe vilivyo hatarini, CITES, lakini pia mikataba miwili ya Umoja wa Mataifa kuhusu uhalifu wa kupanga unaovuka mipaka, na mkataba dhidi ya rushwa.