Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua zahitajika kushughulikia kutokuwa na utaifa kwa watoto

Hatua zahitajika kushughulikia kutokuwa na utaifa kwa watoto

Watoto wasio na utaifa kote duniani wana hisia zinazofanana za kubaguliwa, kuvunjika moyo na kukata tamaa, kwa mujibu wa ripoti mpya ya Shirika la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR.

Kwa mantiki hiyo, UNHCR imeonya kuwa hatua za dharura zinahitajika kabla kutokuwa na utaifa kuyaweke maisha ya watoto hao katika jinamizi ya taabu.

Ripoti hiyo ambayo imetokana na maoni yaliyokusanywa kutoka kwa watoto wasio na utaifa katika maeneo mengi, imesema kuwa mengi ya matatizo wanayokumbana nayo watoto hao katika nchi kulikofanywa utafiti, huathiri jinsi wanavyofurahia utoto wao, kuishi maisha yenye afya, pamoja na kusoma na kutimiza azma yao katika maisha.

Kamishna Mkuu wa UNHCR, António Guterres, amesisitiza kuwa ripoti hiyo ambayo imetolewa mwaka mmoja baada ya kuzinduliwa kwa kampeni ya kutokomeza kutokuwa na utaifa ifikapo mwaka 2024 iitwayo #IBelong, inamulika haja ya kukomesha taabu ya watoto wanaokosa utaifa katika dunia ambapo mtoto mmoja huzaliwa bila utaifa kila dakika kumi.