Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uchaguzi Côte d'Ivoire, Ban ampongeza Ouattara kwa kuchaguliwa tena

Uchaguzi Côte d'Ivoire, Ban ampongeza Ouattara kwa kuchaguliwa tena

Hatimaye baraza la kikatiba nchini Côte d'Ivoire limetangaza matokeo ya uchaguzi wa rais uliofanyika nchini humo tarehe 25 mwezi uliopita ambapo Rais Alassane Ouattara amechaguliwa kuongoza tena nchi hiyo.

Kufuatia matokeo hayo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amempongeza Rais Ouattara sambamba na wananchi na serikali ya Côte d'Ivoire kwa hitimisho la uchaguzi huo lililokuwa na mafanikio.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amemnukuu Ban akipongeza tume huru ya uchaguzi nchini humo kwa maandalizi mazuri yaliyowezesha uchaguzi huo kufanyika kwa ueledi mkubwa na kwa misingi ya katiba ya Côte d'Ivoire bila kusahau taasisi za kiraia..

(Sauti ya Dujarric)

“Katika Mkuu ametambua mahsusi kabisa kazi nzuri ya ushiriki wa wa taasisi za kiraia ambao amesema umechangia uwazi na uhalali wa uchaguzi huo.”

Katibu Mkuu amesema ni matumaini  yake kuwa mwenendo wa uchaguzi huo umethibitisha jinsi Côte d'Ivoire inavyorejea katika kuwa na amani ya kudumu na kupongeza uongozi wa nchi hiyo na wananchi wake walivyojitoa bila kuchoka katika kipindi cha miaka mitano kuimarisha amani, kuendeleza demokrasia na utawala wa kisheria.

Amesema anaamini kuwa mwelekeo uliojitokeza wakati wa uchaguzi wa Rais utakuwa vivyo hivyo wakati wa uchaguzi wa wabunge na kwamba Umoja wa Mataifa unatarajia kushirikiana na Rais Ouattara na wananchi katika kuainisha majukumu ya Umoja huo katika kuimarisha amani, utulivu na demokrasia.