Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban aeleza kusikitishwa na chuki inayoenezwa Myanmar

Ban aeleza kusikitishwa na chuki inayoenezwa Myanmar

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ameeleza kusikitishwa na maneno ya chuki, uchochezi wa uhasama wa kijamii na matuimizi ya dini kwa sababu za kisiasa miongoni mwa jamii ya walio wengi nchini Myanmar.

Kwa mantiki hiyo, Katibu Mkuu amesema kuwa amezingatia uhasimu ulioonyeshwa dhidi ya mashirika ya kimataifa, ikiwemo Umoja wa Mataifa, na kulaani hasa matusi yaliyoelekezwa kwa mtaalam maalum wa Umoja huo anapofanya kazi yake, ikiwa siyo mara ya kwanza.

Taarifa ya msemaji wake imesema Ban ana wasiwasi kuwa ukwepaji sheria unaoendelea licha ya tabia hizo huenda ukaathiri sifa ya Myanmar kimataifa.

Taarifa hiyo pia imesema kuwa Katibu Mkuu amepeleka barua kwa Rais U Thein Sein, akielezea Imani yake na uungaji mkono wake kwa kazi muhimu anayofanya Mtaalam maalum wa haki za binadamu, Yanghee Lee.

Wakati uchaguzi ukikaribia Novemba 8, ametoa wito kwa wadau wote Myanmar kujiepusha na shinikizo au vitisho vyovyote,  kueneza chuki au machafuko dhidi ya watu binafsi au mashirika kwa misingi ya kabila, jinsia, dini au mitazamo ya kisiasa.