Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban akaribisha matokeo ya mkutano wa Geneva kuhusu Syria

Ban akaribisha matokeo ya mkutano wa Geneva kuhusu Syria

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amekaribisha matokeo ya mkutano uliofanyika mnamo Oktoba 30, 2015 kuhusu Syria mjini Vienna, Austria, na kuwapa heko washirika, hususan Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergey Lavrov kwa uongozi, ahadi na kujituma kwao.

Taarifa ya msemaji wake imemnukuu Katibu Mkuu akisema kuwa, kama walivyokiri washirika kwenye mkutano huo wa Vienna, bado kuna tofauti kubwa. Taarifa hiyo imeenda mbalio zaidi ikisema Katibu Mkuu anatumai kuwa katika siku na wiki zijazo, watazipunguza tofauti hizo na kujenga fursa za makubaliano.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Ban amesema watu wa Syria wameteseka kwa muda mrefu. Kwa mantiki hiyo, ametoa wito kwa serikali ya Syria na upinzani kuchukua hatua zote ziwezekanazo ili kuunga mkono mlango uliofunguliwa kwa makubaliano ya Vienna ili kuumaliza mzozo ulioighubika nchi hiyo. Ban ameahidi uungaji mkono wa Umoja wa Mataifa kikamilifu katika kuusongesha mchakato wa mazungumzo ya amani mbele.